Steel Dome: Ufahamu mfumo hatari wa ulinzi wa Uturuki
Mfumo wa ulinzi wa anga wa "Steel Dome" wa Uturuki ni mfumo changamano ulioundwa maalumu kwa ajili ya ulinzi dhidi ya vitisho vya anga kutoka maeneo yote.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameuita mfumo huu kama "mfumo wa mifumo," akisisitiza uwezo wake wa kuunganisha viwango tofauti vya ulinzi wa anga.
Mfumo huu umeundwa kuunganisha tabaka zote za mitandao ya ulinzi wa anga, na kuunda picha kamili ya anga inayopitisha data moja kwa moja kwenye kituo cha operesheni. Unatajwa kama mfumo imara na hatari kwa adui anayeshambulia kwa njia ya anga.
Maamuzi ndani ya mfumo huu hufanywa kwa kutumia akili mnemba (AI). Mfumo huu wa "Steel Dome" umetengenezwa kutumika ndani na nje ya Uturuki.
Maoni ya wataalam
Wataalam wamechunguza muda, umuhimu, na sifa za mfumo huu. Wanabainisha kuwa vifaa vya ulinzi vinavyotengenezwa na Uturuki vinaweza kufanya kazi kwa ushirikiano.
Sinan Ulgen, mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa uchumi na sera za kigeni, ameelezea mwelekeo wa Uturuki katika mkakati wa ulinzi wa anga kama "njia sahihi."
Anaona mpango huu kama "mradi wa kiwango cha juu," na kwamba ni mfumo wa ulinzi jumuishi wa Uturuki, ukichukua jukumu la kuongoza katika uwekezaji wa ulinzi wa anga.
Aaron Stein, mtaalam wa ulinzi wa Marekani anayefuatilia kwa karibu maendeleo ya kifaa hiki nchini Uturuki, ameeleza kuwa mradi huo umeundwa kukabiliana na "vitisho mbalimbali kutoka kwa makombora tofauti."
Umuhimu wa "Steel Dome"
Umuhimu wa "Steel Dome" unatokana na uwezo wake wa kuunganisha mifumo tofauti ya ulinzi na kutoa jibu la kina dhidi ya vitisho mbalimbali vya anga.
Tukio la hivi karibuni la vita kati ya Israeli na Iran limethibitisha umuhimu mkubwa wa mifumo ya ulinzi wa anga.
Rais Erdogan alisisitiza kuwa "kuwa na makombora yenye ukubwa tofauti na kufanya kazi pamoja kama seli katika mwili ni muhimu sana," akisisitiza haja ya kuongeza uwezo wa silaha za ardhini.
Je, unafanana na "Iron Dome" ya Israel?
Sinan Ulgen amesema kuwa "wazo hili lilitekelezwa ulimwenguni na Israeli, ambapo wao Israel wamekuja na mfumo wa Iron Dome."
Hata hivyo, Aaron Stein amefafanua kuwa mifumo hii ni mifumo viwili tofauti. "Mfumo wa Uturuki umeundwa kwa ajili ya matumizi ya ulinzi wa anga dhidi ya ndege na makombora," wakati Iron Dome ya Israeli imejikita zaidi katika kukabiliana na makombora ya masafa mafupi na roketi.
Je, Uturuki inatumia mfumo wa S-400?
Kufuatia uzinduzi wa mfumo wa "Steel Dome," mjadala umeibuka kuhusu makombora ya S-400 ambayo Uturuki ilinunua kutoka Urusi.
Murat Yatkin ameeleza kuwa, kutokana na uanachama wa Uturuki katika NATO, kuunganisha S-400 na "Steel Dome" kunaweza kuwa na matatizo.
Sinan Ulgen pia amebainisha kuwa uendeshaji na matengenezo ya vifaa vya S-400 vinahitaji wataalam wa Urusi.
Uturuki ilinunua S-400 kutoka Urusi mwaka 2017 kwa dola bilioni 2.5, na uwasilishaji wake ulichukua hadi mwaka 2019. Wakati Uturuki iliponunua vifaa hivi, Marekani iliweka vikwazo na Ankara ilinyimwa kufanya biashara ya ndege za kivita za kizazi cha tano za F-35.
"Steel Dome" itaaza kufanya kazi lini?
Ulgen amesema kuwa mfumo wa "Steel Dome" sasa unaweza kutumika kujilinda dhidi ya makombora ya masafa ya kati, na kazi tayari umeanza.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mfumo bado haujakamilika vyema, kwani Uturuki itaendelea kutumia vifaa vingine vya ulinzi. Ameongeza, "Kuendeleza mfumo wa ulinzi unaofunika nchi nzima, kuupima, kubaini mafanikio yake, na kisha kuufanya kuwa kifaa kinachotegemewa kwa kawaida huchukua muda."
Jeshi la Uturuki kwa sasa lina mfumo wa makombora ya kutungua vifaru wa Aselsan uliotengenezwa Uturuki kwa miinuko ya chini na mifumo ya makombora ya kutungua ndege ya Hisar.
Vifaa hivi vinatarajiwa kuwasilishwa kwa wanajeshi kufikia mwisho wa mwaka huu.