Bunge lahitimishwa - Je, 'No Reforms' ya Chadema imezikwa rasmi?
Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekamilisha rasmi shughuli zake tarehe 27 Juni 2025 kwa Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia. Bunge hilo litavunjwa rasmi Agosti 03, 2025 litakapokamilisha kipindi chake kikatiba. Baada ya hatua hiyo itafungua rasmi dirisha la kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025. Katika uchaguzi huo, Watanzania watawachagua madiwani, wabunge, na Rais.

Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Tundu Lissu, kimeendelea kushikilia msimamo wa kupigania mageuzi ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi kufanyika. Kupitia vuguvugu yao maarufu ya No Reforms No Election, CHADEMA kinadai kuwepo kwa mazingira huru, haki, na sawa ya uchaguzi.
Katika kauli yake, Lissu alisema: "Tunataka mabadiliko ya mfumo wetu wa uchaguzi. Hatutaki mfumo utakaoipendelea CHADEMA au unaoipendelea CCM, tunataka mfumo ulio huru."
"Kupiga kura hakuna maana tena, kura haina thamani yoyote kuamua mwenyekiti, diwani, mbunge au rais. Tumechoka kudhulumiwa kweli, tupiganie mabadiliko, tusisimamiwe uchaguzi na mfumo huu," alisema Lissu akiwa Iringa siku chache kabla ya kukamatwa kwa tuhuma za uhaini.
Mabadiliko yanayotakiwa na CHADEMA
Pamoja na vyama vingine kama ACT-Wazalendo, CHADEMA imekuwa ikisisitiza haja ya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi, ambayo ni pamoja na:
- Kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi inayojitegemea kweli
- Uchaguzi usisimamiwe na wakurugenzi wa halmashauri
- Wagombea kupita bila kupingwa
- Ushiriki wa wagombea usizuiwe kwa sababu zisizo za msingi
- Kuwepo kwa mazingira ya usawa kwa mawakala wa vyama
- Matokeo ya urais yaweze kuhojiwa mahakamani
- Kuzuia kura feki na vituo hewa
- Vyombo vya ulinzi visiingilie uchaguzi