Maandamano 7 yaliyowahi kutikisa Afrika
Maandamano yamekuwa silaha muhimu sana barani Afrika, yakitumika na raia kuonyesha kutoridhika, kudai haki, na kushinikiza mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijamii.

Kuanzia mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi hadi kudai utawala bora na haki za kiuchumi, maandamano haya yameacha alama kubwa isiyofutika kwenye historia ya bara hili.
Juni 25, 2025 ni mwaka mmoja tangu maandamano yaliyoongozwa na vijana yalipofanyika nchini Kenya wakipinga Muswada wa Fedha 2024 na uongozi mbovu.
Wakati vijana hao maarufu kama Gen Z wa Kenya wakiendelea na maandamano kila wakati kwa sababu tofauti, ikiwemo ya kuazimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya mwaka uliopita, ni muhimu kukumbuka baadhi ya matukio sita makuu ya kihistoria yaliyotikisa Afrika na kubadili mkondo wa matukio, huku tukiangalia pia athari zake za kibinadamu.
1. Maasi ya Soweto, Afrika Kusini (1976)
Maasi ya Soweto yalianza Juni 16, 1976, yakiongozwa na wanafunzi weusi wa shule za Sekondari waliopinga vikali amri ya serikali ya kibaguzi ya kuanza kutumikwa kwa lugha ya Kiafrikana kama lugha ya kufundishia kwa shule za watu weusi.
Lugha ya Kiafrikana ilionekana kama nembo ya ukandamizaji wa kibaguzi, na wanafunzi waliona amri hiyo kama unyanyasaji wa kitamaduni na kielimu.
Maandamano hayo, yaliyoanza kwa amani, yaligeuka kuwa umwagaji damu mkubwa. Polisi walikabiliana na waandamanaji aidi ya 20,000 kwa risasi za moto, na kusababisha vifo vya mamia ya wanafunzi na majeruhi elfu kadhaa. Takwimu zinasema waliuawa watu 176, lakini zingine zinasema ni wengi kufikia 700.
Picha ya Hector Pieterson, mvulana wa miaka 13 aliyepigwa risasi na kuuawa, ilisambaa duniani kote na kuamsha hasira kubwa kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi (Apartheid), na hatimaye kuchangia kuanguka kwa utawala huo wa kikatili. Mpaka leo Juni 16 kila mwaka ni siku ya mapumziko taifa hilo likiazimisha sikju ya vijana kuheshimu kilichotokea Soweto.
2. Vuguvugu la Ukombozi la Angola na Msumbiji (1960 - 1970)
Maandamano na mapambano ya ukombozi nchini Angola na Msumbiji yalikuwa mifano ya wazi ya jinsi wananchi walivyotumia nguvu ya umma kupinga utawala wa kikoloni wa Ureno.
Raia walichoshwa na ukandamizaji, ubaguzi wa rangi, na kunyimwa haki za kisiasa na kiuchumi. Maandamano ya awali, migomo, na maandamano ya kiraia yalikandamizwa kikatili, na kusababisha vifo na mateso kwa wananchi wengi.
Ukandamizaji huu ulisababisha kuibuka kwa makundi yenye silaha kama vile MPLA nchini Angola na FRELIMO nchini Msumbiji, yaliyoanzisha vita vya msituni.
Mapigano haya yalichukua miaka mingi na kusababisha maelfu ya vifo, uharibifu mkubwa wa miundombinu, na mamilioni ya wakimbizi.
Mafanikio ya harakati hizi yaliashiria mwisho wa utawala wa kikoloni wa Ureno barani Afrika na kuwa kielelezo cha uhuru kwa mataifa mengine.
3. 'Jasmine Revolution' - Tunisia (2010-2011)
Maandamano haya yalilipuka kati ya Disemba 17, 2010 mpaka 14 Januari 2011 kufuatia kujichoma moto kwa Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga, aliyelalamikia unyanyasaji wa polisi na ukosefu wa fursa za kiuchumi.
Kitendo chake kilizua ghadhabu kubwa na kusababisha maandamano makubwa kote nchini, yakidai mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, pamoja na kuondolewa kwa rushwa na ukosefu wa ajira.
Serikali ilijaribu kuzuia maandamano hayo kwa nguvu, na kusababisha vifo vya waandamanaji kadhaa na majeruhi wengi, lakini shinikizo la umma lilikuwa kubwa mno. Taarifa zinasema watu 338 waliuawa na wengine 2,174 kujeruhiwa.
Ndani ya wiki chache tu, Rais Zine El Abidine Ben Ali, aliyekuwa madarakani kwa miaka 23, alikimbia nchi. Mapinduzi ya Tunisia yalienea kwa kasi kote Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati, yakijulikana kama "Arab Spring" (Chemchemi ya Kiarabu), na kusababisha maandamano makubwa na mabadiliko ya kisiasa katika nchi kadhaa.
4. Maandamano ya mapinduzi ya Januari 25
Mapinduzi ya Januari 25 nchini Misri yalianza kwa kasi Januari 2011, yakichochewa na machafuko ya kisiasa na kiuchumi yaliyotikisa Tunisia na kwingineko Mashariki ya Kati. Maelfu ya Wamisri walijitokeza katika Uwanja wa Tahrir Square, Cairo, wakidai mageuzi ya kisiasa na kumwondoa Rais Hosni Mubarak, ambaye alikuwa madarakani kwa miaka 30. Maandamano hayo yalianza kama wito wa amani lakini yalikutana na ukandamizaji mkali kutoka kwa vikosi vya usalama.
Licha ya upinzani wa mabomu ya machozi, risasi za mpira, na hata risasi za moto kutoka kwa Polisi, waandamanaji hawakuvunjika moyo. Takriban watu 846 waliuawa na zaidi ya 6,000 kujeruhiwa katika mapigano hayo, lakini vifo na majeraha viliamsha hasira zaidi na kuongeza idadi ya washiriki mitaani.
Baada ya siku 18 za maandamano yasiyokoma, hatimaye Februari 11, 2011, Hosni Mubarak alitangaza kujiuzulu, akikabidhi mamlaka kwa baraza la kijeshi. Kujiuzulu kwake kulisababisha sherehe kubwa za ushindi katika Tahrir Square na kote Misri, kukiashiria mwisho wa utawala wa kidikteta na kuonesha nguvu kubwa ya umma katika kudai mabadiliko.
Ingawa Misri ilikabiliwa na changamoto nyingi baada ya tukio hilo, Maandamano yaliyoleta mapinduzi ya Januari 25 yamebaki kuwa kielelezo muhimu cha mapambano ya demokrasia barani Afrika na duniani.
5.Maandamano ya kumng'a Omar al-Bashir - Sudan (2018-2019)
Kuanzia Desemba 2018, maelfu ya Wasudan waliingia mitaani kupinga kupanda kwa bei za mkate na mafuta, lakini haraka maandamano hayo yalibadilika na kuwa wito wa kuuangusha utawala wa Rais Omar al-Bashir.
Maandamano haya yaliendelea kwa miezi kadhaa, yakiongozwa na Chama cha Wataalamu wa Sudan (SPA) na kuungwa mkono na makundi mbalimbali ya kiraia, yakihitaji kuondolewa kwa serikali iliyokuwa madarakani kwa miaka 30.
Licha ya ukandamizaji mkali kutoka kwa vikosi vya usalama, ambapo mamia ya waandamanaji waliuawa na maelfu kujeruhiwa, shinikizo la umma lilikuwa kubwa kiasi kwamba mnamo Aprili 2019, jeshi la Sudan lilimpindua al-Bashir.
Maandamano haya yalionesha wazi nguvu ya raia katika kufanya mabadiliko makubwa hata katika mazingira ya ukandamizaji mkali. Hata hivyo zaidi ya waandamanaji 100 walielezwa kufariki dunia.
6. Maandamano ya #FeesMustFall - Afrika Kusini (2015-2016)
Vuguvugu la #FeesMustFall lilianza mwaka 2015 likiongozwa na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini waliopinga ongezeko la ada za masomo.
Maandamano haya yalienea haraka kote nchini, yakishuhudia migomo, vizuizi vya barabara, na hata mapigano makali na polisi.
Kulikuwa na ripoti za majeruhi kadhaa miongoni mwa wanafunzi na kukamatwa kwa wengi. Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha elimu ya juu inapatikana kwa wote, hasa kwa wale kutoka familia masikini, na kupinga utofauti uliokuwepo bado baada ya kumalizika kwa 'Apartheid'.
Ingawa haikufuta ada zote, vuguvugu hili lilishinikiza serikali kutoa ruzuku zaidi kwa wanafunzi na kuanza majadiliano juu ya elimu isiyo na ada, likisisitiza tena umuhimu wa sauti ya vijana katika siasa za nchi. Yalikuwa moja ya maandamani yaliyokuwa na nguvu na kukusanya watu wengi mtaani.
7.Maandamano ya mswada wa fedha - Kenya (2024)
Maandamano ya hivi karibuni nchini Kenya yaliyojulikana kama "Reject Finance Bill" au "Occupy Parliament" yalianza Juni 2024, yakiongozwa na vijana wengi kupitia mitandao ya kijamii, kupinga mswada wa fedha uliopendekeza kodi mpya na kuongeza kodi zilizopo.
Maandamano haya ya Gen Z yalienea haraka nchi nzima na kushuhudia waandamanaji wakijitokeza kwa wingi mitaani, wakitumia ubunifu na teknolojia kuandaa na kuratibu. Licha ya polisi kujaribu kukabiliana nao, ambao umesababisha vifo vya waandamanaji kadhaa na mamia ya majeruhi pamoja na kukamatwa kwa wengi, maandamano hayo yalifanikiwa kushinikiza serikali kuondoa sehemu kubwa ya mswada huo, na hatimaye kuufuta mswada mzima.
Haya yamekuwa maandamano yenye nguvu ya kuonyesha jinsi vijana, wakitumia mitandao ya kijamii, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi.